News Archive


Shirika la Taifa la hifadhi ya Jamii (NSSF) limetoa mkopo wa Tshs bilioni 8.99 kwenda kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ya Tanzania kwa ajili ya ufufuaji wa kiwanda cha usindikaji wa nafaka katika jiji la Mwanza  ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za NSSF kutekeleza kwa vitendo sera ya uchumi wa viwanda hapa nchini.

 

Mkopo huu unalenga kuiwezesha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuweza kuvifufua vinu vyake viwili vya usindikaji wa mazao ya mpunga na mahindi vilivyopo mkoani Mwanza kwa  kununua vifaa na mitambo mipya na hatimaye kuanza uzalishaji baada ya kusimamisha uzalishaji huo mapema miaka ya 1990.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya hundi ya mkopo huo iliyofanyika tarehe 20 Agosti 2017 jijini Mwanza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Jenista Mhagama alitoa wito kwa Wizara yenye dhamana ya kilimo hapa nchini kuisimamia vyema bodi hiyo kiutendaji ili iweze kujiendesha kwa ufanisi utakaoiwezesha kurejesha mkopo huo unaotarajiwa kulipwa ndani ya kipindi cha miaka sita (6) ikijumlisha kipindi cha mpito yaani (grace period) ya mwaka mmoja.

Waziri Mhagama akikabidhi hundi hiyo kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba (kushoto) huku wadau wengine wakishuhudia

"Mbali na Wizara yenye dhamana ya kilimo, pia niwaombe sana uongozi wa mkoa wa Mwanza chini ya Mkuu wa mkoa kutambua kuwa ufanisi wa kiwanda hiki unategemea sana uwepo wa malighafi ya kutosha hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha uwiano kati ya uzalishaji wa malighafi na uzalishaji wa kiwanda vinakwenda sambamba,'' alisisitiza.

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Bw Stanislaus Mabula akitoa shukrani zake kwa  niaba ya wananchi wa jimbo hilo pamoja na wakazi wa Mwanza kwa ujumla

Mh. Jenista Mhagama alilipongeza Shirika la NSSF  kwa uwekezaji wa viwanda vyenye tija kiuchumi ndani ya muda mfupi ambapo kwa kipindi cha takriban mwaka mmoja uliopita hadi sasa shirika la NSSF limewekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kiwanda cha kutengeneza viuadudu vya kuua vimelea vya mbu kiitwacho Tanzania Biolarvicide Limited kilichopo Kibaha, mkoani Pwani.

Waziri Mhagama, Mbunge Stanislaus Mabula na wadau wengine wakitembelea eneo la kiwanda ambapo ndipo kitakapojengwa kinu cha kusagia mahindi chenye uwezo wa kusaga mahindi hadi kufikia tani 250 kwa siku.

"Uwekezaji wa NSSF pia unaonekana kwenye bodi ya nafaka na Mazao mchanganyiko ya Tanzania, Mkoani Dodoma, viwanda vipya vya kuzalisha sukari Mkulazi, mkoani Morogoro, kiwanda cha chaki Maswa (Maswa Chalk & General Enterprises) ambacho kipo Simiyu.hongereni sana!'' alipongeza Mh. Mhagama

Muonekano wa sehemu ya mitambo ya  kiwanda cha kukobolea mchele kilichopo wilayani Nyamagana jijini Mwanza

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alimuhakikishia Waziri Mhagama kuwa mbali na kuisimamia kwa ukaribu bodi hiyo ili iweze kurejesha mkopo huo, wizara yake imejipanga kuhakikisha kwamba miradi yote ya kilimo inayohusisha uwekezaji kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii hapa nchini inasimamiwa kwa umakini, ufanisi na weledi mkubwa ili kulinda pesa ya wanachama wa mifuko hiyo.

"Kwa kutambua kwamba ufanisi wa viwanda hivi unategemea zaidi kilimo kuna mipango na mikakati mizuri kuhakikisha mnyororo wa thamani unaohusika kuzalisha malighafi za viwanda hivi haukatiki,'' alisema Waziri Tizeba.

Mapema, akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi mkuu wa NSSF Prof.Godius Kahyarara alisema kuwa mbali na lengo la kutunza thamani ya michango ya wanachama, uwekezaji unaofanywa na shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii pia unalenga kuchochea ukuaji wa shughuli mbali mbali za uchumi na kijamii ambazo pia huongeza ajira, kipato na kuinua kiwango cha maisha ya watanzania walio wengi na mwishowe kuongeza wanachama wa mfuko.

"Mkopo huu utapelekea kufufua kiwanda ambacho kitaleta ajira Zaidi ya 340 za moja kwa moja na ajira zaidi ya 23,000 ambazo hazitakuwa za moja kwa moja.Hii itachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania na pia kuongezeka kwa wanachama wa Mfuko,'' alibainisha.

Prof.Kahayrara alisisitiza kuwa Uwekezaji huo unafanywa kwa  kuzingatia Sera ya Uwekezaji ya Shirika na Mwongozo wa Uwekezaji kwa Mashirika ya Hifadhi ya Jamii unaotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kushirikiana na Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).

Akitoa taarifa za kiwanda hicho,Mtendaji mkuu wa  bodi ya nafaka  na mazao mchanganyiko ndugu  John Maige alisema  mkopo huu utaongeza kiwango cha usagaji wa mahindi hadi kufikia tani 250 kwa  siku na ukoboaji wa tani 96 za mchele kwa siku pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa vyakula vya mifugo kwa Masoko ya ndani na nje ya nchi.

Mtendaji mkuu wa  bodi ya nafaka  na mazao mchanganyiko Bw. John Maige akifafanua mradi huo

"Mkopo huu pia utawezesha kuwepo kwa soko la uhakika kwa wakulima wa mahindi na mpunga hapa nchi na nitumie fursa hii kuipongeza serikali kwa hatua ya kuzuia usafirishaji wa mazao ghafi nje ya nchi.'' alipongeza Maige huku akiongeza shukrani zake kwa Mfuko wa NSSF kwa uamuzi wa kuwekeza kwenye kufufua kiwanda hicho.

Frequently Asked Questions

 • Nawezaje kuwa mwanachama wa NSSF? +

  Tafadhali fika katika ofisi yoyote ya NSSF iliyo karibu yako kwa zoezi la uandikishaji ukiwa na picha moja ya passport Read More
 • Napataje taarifa ya Michango yangu? +

  Kupata taarifa ya Michango, unafanya ifuatavyo : a) Sajili Tuma neno sajili,acha nafasi, weka namba yako ya uanachama. Tuma kwenda namba Read More
 • Je nifanyeje endapo michango yangu haionekani katika taarifa za akaunti yangu? +

  Tafadhali fika ofisi ya NSSF iliyo karibu nawe ili kujua sababu ya kutoonekana kwa michango yako na kuelekezwa utaratibu wa Read More
 • Je narekebishaje michango yangu? +

  Michango ya mwanachama itarekebishwa kulingana na sababu zinazopelekea kutoonekana kwa michango hiyo katika taarifa ya michango. Ofisi husika itakupa muongozo zaidi. Read More
 • Je mwanachama anayesafiri anaweza kumwachia mtu au ofisi imfatilie madai na kuchukua malipo yake?? Kwa utaratibu gani?? +

  Ndio, mwanachama anaruhusiwa kwa kujaza fomu za mandate (NSSF 22) zilizothibitishwa na mwanasheria na kufata taratibu zote za kisheria zilizoainishwa Read More
 • 1
 • 2
 • 3
 • 4