emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

ERIO ARIDHISHWA NA HUDUMA ZINAVYOTOLEWA KWA WANANCHI KATIKA BANDA LA NSSFMKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) William Erio, amefurahishwa na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi wanaotembelea banda la NSSF katika maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Erio alitembelea jana banda la mashirikiano kati ya NSSF na PSSSF na kushuhudia wananchi mbalimbali waliotembelea banda hilo namba 13 jinsi wanavyopatiwa huduma mbalimbali kwa haraka bila ya kupoteza muda.

Miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na wananchi kujiunga na NSSF kupitia Mfumo wa Taifa wa Sekta isiyo rasmi na kupewa kadi za uanachama papo hapo muda mfupi baada ya kujiunga.

Huduma nyingine zinazotolewa na NSSF kwa wanachama wanaotembelea banda hilo ni taarifa za michango yao inayowasilishwa na waajiri wao kama ni sahihi.

Aidha, wananchi na wanachama wanapata elimu kuhusu mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF; Ikiwa ni pamoja na namna wanavyoweza kupanga au kununua nyumba za Kijichi kupitia mpango wa mnunuzi mpangaji.

Vile vile, Mkurugenzi Mkuu Erio alishuhudia namna Mifumo ya Tehama inavyo muondolea usumbufu mwanachama wa NSSF ambapo sasa halazimiki kufuata huduma kwenye ofisi za Shirika hilo badala yake anaweza kuona taarifa zake kupitia simu yake ya kiganjani.

Halikadhalika, Kutokana na maboresho hayo ya mifumo mwanachama anaweza kuona taarifa zake kupitia kompyuta mpakato au tovuti ya Shirika ambayo ni www.nssf.or.tz.