emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

WANANCHI TEMBELEENI BANDA LA NSSF TUWAHUDUMIE


WANANCHI wametakiwa kutembelea banda la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili wapate elimu mbalimbali kuhusiana na mafao yanayotolewa na Shirika hilo na kufahamu haki zao pindi wanapostaafu kazi au kukutwa na janga lolote wanapokuwa kazini.

Hayo yalisemwa jana na Mameneja mikoa wa Ilala, Temeke na Kinondoni mara baada ya kutembelea banda namba 13 la ushirikiano la NSSF na PSSSF lililopo katika maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).


Maneja wa NSSF Mkoa wa Ilala, Jacob Sulle, alisema huduma zinazotolewa kwenye ofisi za Shirika hilo ndio zinazotolewa Sabasaba, na kwamba hivi sasa NSSF imeboresha huduma zake hasa kwa wanachama wao kwa maana wanapata huduma kiganjani bila ya kufika ofisini.

"Hivi sasa mwanachama anaweza akapiga simu kwenye 'call center' yetu akapata huduma kama vile ametembelea ofisi za NSSF," alisema Sulle.


Alisema mwanachama anaweza akaangalia salio lake kupitia simu yake ya mkononi kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwa kuandika neno NSSF salio, halafu akaweka namba yake ya uanachama na kuituma kwenda namba 15200.


Kuhusu ulipaji mafao, Sulle alisema hivi sasa NSSF wanalipa mafao ya wanachama wao kupitia 'online' na mwanachama anapata SMS itakayo msaidia kuona kitu alicholipwa.

Alisema lengo la kuboresha huduma zao ni kuhakikisha mwanachama haitaji kuandikiwa hundi au kuuliza salio badala yake atalipwa mafao yake kwa wakati na atayaona kwenye akaunti yake ya benki na Shirika litamtumia ujumbe mfupi (sms) kwenye simu yake.


Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Temeke, Rebule Maira alisema Shirika linatoa huduma mzuri kwa wananchi wanaotembelea Sabasaba ikiwemo elimu kuhusiana na mafao yanayotolewa na NSSF.

Alisema hivi sasa baada ya mabadiliko ya sheria NSSF inahudumia Sekta rasmi na Sekta isiyokuwa rasmi, ambapo wanachama wengi waliofurika katika banda hilo wanapenda kufahamu haki zao mbalimbali ambazo zinawekwa na waajiri ili kuwawezesha kupata mafao pindi wanapofikia umri wa kustaafu.


Maira alisema miongoni mwa kero wanazokumbana nazo ni waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati, hivyo aliwataka waajiri wote kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati kama sheria inavyosema.

Naye Meneja wa NSSF Mkoa Kinondoni, Joseph Fungo alisema kuna baadhi ya waajiri ambao hawajawasilisha michango ya wafanyakazi wao NSSF hivyo wanaendelea kutoa elimu kwa waajiri kuhusu umuhimu wa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati.

"Tunawataka waajiri wote ambao hawajawasilisha michango ya wafanyakazi wao kufika kwenye ofisi zetu ili walipe madeni ya michango waliyoiimbikiza kwa kipindi kirefu," alisema.


Alisema ni kosa kisheria mwajiri kulimbikiza madeni ya michango ya wafanyakazi wake hivyo aliwataka wanachama kutembelea banda la NSSF lililopo Sabasaba ili aweze kufahamu michango yake au kutoa taarifa za mwajiri ambaye hajampelekea michango.

Fungo alisema jukumu la NSSF ni kuhakikisha michango ya mfanyakazi inawasilishwa katika Shirika hilo kama sheria inavyosema ili mwanachama anapostaafu mafao yake yatoke kwa wakati.